Wednesday, July 27, 2016


Kwa Jumuiya ya Watanzania, NorwayKILIMANJARO DIASPORA AKAUNTI KATIKA BENKI YA AMANA

Tunapenda kuwafahamisha kuwa Ubalozi umepokea barua kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifahamisha kuhusu Akaunti Maalumu ilioanzishwa na Benki ya Amana kwa ajili ya Diaspora (Kilimanjaro Diaspora Account). Akaunti hiyo inaendeshwa kwa kufuata miongozo ya Dini ya Kiislamu (Sharia Compliance: Al Wadiah na Mudharabah contracts).

Ubalozi utatumika kuthibitisha nyaraka za kufungulia Akaunti (Verification of Documents) zitakazowasilishwa na wanaoishi eneo husika la uwakilishi kabla ya kuendelea na taratibu nyingine za kufungua akaunti hiyo. Uthibitisho huo ni muhimu kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kifedha nchini Tanzania.

Diaspora watakaopenda kufungua akaunti hiyo wanashauriwa kupakua  (download) fomu za kufungulia akaunti kupitia


na wakimaliza kujaza fomu hizo na kupitishwa na Ubalozi watatakiwa kuzituma kwa gharama zao kwenda anuani ya benki kwa njia za DHL, FedEx, EMs.

Wafunguaji wa akaunti wanaweza pia kuwasiliana na Benki ya Amana kwa simu namba +255 22 2129007  au kuongea moja kwa moja na Bw. Dasu Mussa, Meneja wa Masoko na Miradi (+255 786 687 832) au Bw. Muhsin Muhamed, Mkuu wa Kitengo cha Uzalishaji na Sharia (+255 653 283 636).

Ubalozi wa Tanzania
SWEDEN 


Monday, July 04, 2016


Mazishi ya Mzee Gunnar Garbo aliyefariki 29.Juni 2016


Taarifa za msiba wa aliyekuwa Balozi wa Norway nchini Tanzania kuanzia 1987 hadi 1992.

Mzee Gunnar Garbo alifariki wiki iliyopita tarehe 29.Juni 2016. 

Mzee Gunnar na mkewe mama Profesa Birgit-Brock Utne wana mapenzi sana kwa Tanzania. 

Mama Birgit amewasaidia wanafunzi wengi wa Kitanzania kwa miaka mingi Chuo Kikuu cha Oslo. Hivi sasa yuko kwenye mradi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar. 

Mazishi yatakuwa siku ya Alhamisi tarehe 7.Julai 2016 kwenye kanisa la Nessoden saa saba mchana. 

Wote mnakaribishwa. 


Mwenyezi Mungu Amlaze Mahali Pema, Ameen.


Wednesday, February 03, 2016

Tunapenda kuwataarifu kuwa mipango ya kuusafirisha mwili wa marehemu, kaka Mikidadi Akida imekamilika.Atasafirishwa Alhamisi, 4.Februari 2016 saa 11 jioni (17:00 CET) tokea uwanja wa ndege Gardemoen Oslo na shirika la ndege Turkish Airlines na watafika Dar es Salaam usiku wa kuamkia Ijumaa majira ya saa 9 za usiku (03:00 EAT). Tunayo fursa ya kuuaga mwili wa marehemu, fursa hio ni kesho pale uwanjani Gardemoen saa 8 mchana (14:00 CET) sehemu ya Cargo kwa atakayeweza.

Tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa wale wote waliofanikisha safari hii na kawatakia safari njema.

Mwenyezi Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi Mzee wetu, kaka Mikidadi Akida.
Amin.

Sunday, January 31, 2016


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

TAARIFA KWA WANANCHI NA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA ZIKA (ZIKA VIRUS)
1. Utangulizi

Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya Kitaifa na Kimataifa kuhusu Homa ya Zika ambao ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama "Zika Virus". Ugonjwa huu uligundulika kwa mara ya kwanza nchini Uganda katika miaka ya 1947 kwenye wanyama aina ya sokwe/nyani (rhesus macaque) ndani ya Misitu ya Zika, karibu na Ziwa Victoria. Mnamo mwaka 1952, ugonjwa wa zika uligundulika kwa binadamu nchini Uganda na Tanzania, na mwaka 1968 uligunduliwa nchini Nigeria. Kuanzia mwaka 1951 hadi 1981, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi takribani sita (6) za Afrika ambazo ni Afrika ya Kati, Misri, Gabon, Sierra Leone, Tanzania na Uganda. Vile vile, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa katika nchi za India, Indonesia, Malaysia, Philipine, Thailand na Vietnam na pia nchi za Amerika na Pacific. 

Kuanzia mwezi Mei 2015, ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa ambapo hadi sasa umeathiri zaidi Bara la Amerika ya Kusini. Kuna takribani nchi 22 ambapo Wagonjwa wamethibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa wa Zika. Nchi hizo ni Brazil (Majimbo 14 yameathirika),  Colombia, Suriname, El Salvador, Guatemala, Paraguay, Mexico, Venezuela, Panama, Cape Verde, Honduras, Panama, France (French Guiana na Martinique, United States of America (Puerto Rico), Guyana, Barbados, Ecuador, Bolivia, Haiti, Ujerumani, France (Saint Martin and Guadeloupe na Dominican Republic.  

Ugonjwa huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye (huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana/jioni). Aina hii ya kirusi ipo katika familia ya "Flavirus" ambapo pia wapo virusi vya ugonjwa wa Dengue, Homa ya Manjano (Yellow Fever), Japanese ancephalitis na West Nile Virus. 

Kirusi cha homa ya Zika kama kile cha Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa Aedes aegypti. Mbu huyu anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu, huuma wakati wa mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani majira ya asubuhi na jioni kabla ya jua halijazama.  Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, makopo nk. 

2. Dalili za Homa ya Zika

Dalili za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya Dengue, ambazo ni homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na vile vile kupata vipele vidogo vidogo kama harara (Skin rashes). Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 2 hadi 7 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya Zika. 

Uko uwezekano, ambao haujathibitishwa rasmi, kwamba wakati mwingine wagonjwa wanaweza kupata matatizo katika ubongo (Neurological Complications) na miguu kupooza (Gullein Barre Syndrome), na wajawazito huweza kujifungua watoto wenye ulemavu wa kichwa yaani kichwa kuwa kidogo kulingana na umri wa mtoto (microcephaly).

Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria. Hivyo basi, natoa rai kwa wananchi kuwa, wakati wanapojisikia homa au wamepata homa wahakikishe wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au la, kwa kuwa dalili za ugonjwa wa Zika zinaweza kufanana sana na dalili za malaria.

Homa ya Zika inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna dawa maalum ya ugonjwa huu wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji na damu.

3. Ugonjwa wa Homa ya Zika haujaingia Tanzania 

Mara tu baada ya kuwepo kwa taarifa juu ya ugonjwa huu, Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini pamoja na mipakani kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa (surveillance system ya Wizara).

Tumejiridhisha kuwa ugonjwa wa homa ya Zika kwa sasa haujaingia nchini kwetu. Hivyo, Wananchi wasiwe na hofu ila waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu pamoja na magonjwa ya Dengue na Malaria kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuzingatia yafuatayo:-

(i)  Kuangamiza mazalio ya mbu kwa:

Ø kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.

Ø kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile; vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk. 

Ø kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.

Ø Kuhakikisha kuwa maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.

Ø kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara.

Ø kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.

(ii)  Kujikinga na kuumwa na mbu kwa;-

Ø Kutumia viuatilifu vya kufukuza mbu "mosquito repellants".

Ø Kuvaa nguo ndefu ili kujikinga na kuumwa na mbu.

Ø Kutumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana hasa watoto).

Ø kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.

4. Hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ni pamoja na:-

1. Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inaendelea kuwasiliana na kushirikiana kwa karibu na Shirika la afya Duniani - Ofisi ya Tanzania kwa lengo la kupata Taarifa na maelezo zaidi ya kukabiliana na ugonjwa huu. Kamati ya Dharura ya Miongozo ya Kimataifa ya Afya  ya WHO yaani "International Health Regulations Emergency Committee" itakutana siku ya Jumatatu ya tarehe 1/2/2016, mjini Geneva,Uswisi ili kufanya tathmini ya ugonjwa huo na kutoa tamko na maelekezo zaidi ya namna ya kudhibiti Ugonjwa huu kwa nchi wanachama. 

Baada ya tamko/Mwongozo huo wa WHO, Wizara ya Afya itaandaa Taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kwa ajili ya kusambazwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya Tanzania Bara. Aidha, taarifa hii itajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (ainisho la Ugonjwa), "Ukweli Kuhusu Ugonjwa" (Fact Sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.

2. Wizara itaanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio na Runinga kuhusu ugonjwa huu sambamba pia na ugonjwa wa Dengue ambao uambukizi wake unasababishwa na Mbu aina ya Aedes.

3. Kuendelea kutoa vyandarua vyenye uatilifu katika Mkoa yote Tanzania ili kufikia lengo la asilimia 95.

4. Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa surveillance ya Wizara. Aidha, Wizara inatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya hapa nchini kutoa taarifa za watoto watakaozaliwa wakiwa na ulemavu wowote wa kichwa ikiwemo "microcephaly" au "anencephaly".

5. Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyokuwa ya malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina iwapo kuna ugonjwa huu.

6. Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya Taifa iliyopo katika Taasisi ya uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (Centre for Disease Control (CDC) katika kuhakikisha kuwa vitendanishi vya kutambua ugonjwa huu vinapatikana.

7. Kushirikisha program ya Malaria na NIMR katika kudhibiti mbu kwa kupulizia na kunyunyizia  viuatilifu. Hii inalenga  kuangamiza mbu wapevu na viluwiluwi.

5. Hitimisho

Ugonjwa wa Homa ya Zika bado haujaingia Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya uwepo wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya Zika, Dengue na malaria ambayo huenezwa kwa namna inayofanana.

Aidha, mvua hizi kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini zinaweza kuchangia kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Hivyo, utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka katika vijiji na miji yetu ni lazima uimarishwe katika kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama kwani bila ya kuzingatia hayo, tunatoa fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya binadamu.

Wizara ya Afya itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi ili waweze kuelewa kuhusu ugonjwa huu na kuchukua hatua stahiki.

Imetolewa na:-
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
31/1/2016


Tuesday, January 26, 2016

Tukutane Ijumaa, 29.Januari 2016 kumwenzi Mzee Wetu Mikidadi Akida

 

Chama cha Watanzania Oslo kinawatangazia ndugu, jamaa na marafiki kukutana na kumuenzi mzee wetu na aliyekuwa mmoja wa waasisi wa chama chetu, mzee Mikidadi Akida.

Siku ya ijumaa hii:
Tarehe 29.01.2016.
Kuanzia saa 11 jioni (17:00 CET)
Mahali: NAV Tøyensenteret
Orofa ya 6
Anwani: Hagegata 24

Mnaombwa wote kuhudhuria kwa wingi.

Tunaomba watakaokuja waje na chochote kile cha kula au kutafuna na kinywaji baridi. 

Pia tunaomba tusaidiane kusambaza hii taarifa.

Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi. Amin.

Wenu,
Daddy O. Hassan
Mwenyekiti,
Chama Cha Watanzania Oslo

Monday, December 14, 2015


Thank you!
Asanteni sana!
Kwenu marafiki wa Chama Cha Watanzania Oslo, chama kinapenda kukushukuruni sana kwa juhudi, mshikamano na umoja wenu wa dhati mliouonesha na hatimaye kufanikisha sherehe yetu ya Uhuru wa miaka 54 ya Tanzania Bara. Tuko pamoja sana na tunatarajia ushirikiano wenu kwa shughuli zingenezo zijazo.

Kwa niaba ya Chama Cha Watanzania Oslo, tunashukuru sana.To all of you, friends of 

Chama Cha Watanzania Oslo.  

Tanzanian Organization Oslo would like to thank you for your support and cooperation as well as for being there and celebrate with us for a memorable day of Tanzania Mainland´s 54 years of Independence.
We are together and it´s our hope to be with you for other coming events.

On behalf of Chama Cha Watanzania Oslo,
We say thank you so much!Wednesday, December 09, 2015

TANZANIA MAINLAND (TANGANYIKA) CELEBRATES 54 YEARS OF INDEPENDENCE, 9th.DESEMBER 2015
 The East African nation of Tanzania dates formally from 1964, when it was formed out of the union of the much larger mainland territory of Tanganyika and the coastal archipelago of Zanzibar. The former was a colony and part of German East Africa from the 1880s to 1919, when, under the League of Nations, it became a British mandate until independence in 1961. It served as a military outpost during World War II, providing financial help, munitions, and soldiers. Zanzibar was settled as a trading hub, subsequently controlled by the Portuguese, the Sultanate of Oman, and then as a British protectorate by the end of the nineteenth century. Julius Nyerere, independence leader and "baba wa taifa for Tanganyika" (father of the Tanganyika nation), ruled the country for decades, assisted by Abeid Amaan Karume, the Zanzibar Father of Nation. Following Nyerere's retirement in 1985, various political and economic reforms began.....Monday, November 09, 2015

Rais John Pombe Magufuli amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na amemteua Profesa Lawrence Mseru, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia Jumanne, tarehe 10 Novemba, 2015.


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA   
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website: www.ikulu.go.tz               
Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli , leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.

“Rais  amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko”. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema na kutoa maelekezo yafuatayo :

Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru , kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.

Dkt. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye anayekaimu hivi sasa, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Balozi Sefue pia amesema,   Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.

Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.

Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).

Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.

“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue.

………Mwisho………

Imetolewa na;

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Novemba, 2015