Saturday, November 03, 2007


Na Mrisho Mbogorume, Arusha.

Mrembo wa Arusha 2006/07 Faith Rukio Msuya, ametimuliwa nchini na kuvuliwa taji lake mara tu baada ya Idara ya Uhamiaji nchini kubainika kuwa hakuwa raia wa Tanzania.....

Akizungumza mwandishi wetu mwishoni mwa wiki hii, mmoja wa maafisa wa uhamiaji mkoani hapa aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa madai kuwa hakuwa msemaji wa idara hiyo alisema kuwa, Faith alisharudishwa nchini kwao Kenya miezi kadhaa iliyopita.

“Alirudishwa kwao Kenya baada ya idara hii kubaini kuwa hakuwa Mtanzania na kumtaka arudishe zawadi zote alizopewa katika shindano hilo mara moja kabla ya kuondoka," alisema afisa huyo.

Mwandishi wetu alimtafuta mshindi wa pili wa mashindano hayo, Irene Shirima na kumuuliza kama alishakabidhiwa zawadi baada ya kupokonywa ushindi mshindi wa kwanza Faith, lakini alisema hajapewa.

“Zawadi niliyoambulia ni ya kufanikiwa kuwa Balozi wa Kampuni ya PSI wanaosambaza na kuuza Salama Condom, lakini waandaaji hawajanipa zawadi yangu ambayo ni pesa taslimu shilingi milioni mbili hadi hivi sasa tunavyoongea.

“Sijui nisingekuwa Balozi wa Salama Condom ningeambulia nini? Hiyo ya Faith ndio sijui kama nitapewa au hapana,” alisema Irene.

Aidha, mrembo huyo alitoa wito kwa Kamati ya Miss Tanzania kuwa macho na wandaaji aliowaita kuwa ni ‘feki’ wa mashindano ya urembo katika ngazi za vitongoji kutokana na kutotimiza ahadi wanazowapa washiriki.

Mwandishi wetu alifanikiwa kuongea na mratibu wa Sindano la Miss Arusha 2006/07 aliyejitambulisha kwa jina moja la Lushaka na kusema; Mh! Mambo siyo mazuri mwanangu, uvumilivu unahitajika hadi hapo mambo yatakapotengemaa,” alisema Lushaka.

Shindano la kumsaka mrembo wa Mkoa wa Arusha lilifanyika miezi kaadhaa iliyopita na kushirikisha jumla ya warembo 12 kutoka pande zote la Jiji la Arusha ambapo mshindi wa kwanza alijishindia gari dogo aina ya Toyota lenye thamani ya shilingi milioni 8 na wa pili alijizolea kitita cha shilingi milioni mbili ambao hajapewa hadi sasa huku mshindi wa tatu akiondoka na dishi la DSTV na simu ya mkononi aina ya Nokia.

Kutoka: Global Publishers TZ.

No comments: